KAFULILA ATAKIWA KULIPA MILIONI 7.5 KAMA DHAMANA YA KESI YAKE YA KUPINGA MATOKEO YA UBUNGE
Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) kwa miaka mitano iliyopita, David Kafulila ameamriwa na Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora kulipa Sh7.5 milioni kama dhamana, ili ombi lake lakutaka itengue matokeo ya ubunge wa jimbo hilo yasikilizwe.
Mahakama imetoa uamuzi huo kupitia kwa Jaji Leiyla Mgonya, baada ya kuzingatia maombi ya Kafulila aliyetaka apunguziwe gharama ya fedha za dhamana kutoka Sh5 milioni badala yake alipe Sh1 milioni kwa kila mdaiwa.
Kupitia Wakili wake, Emmanuel Msyani, Kafulila aliwasilisha ombi Mahakama Kuu alipe Sh1 milioni kama dhamana kwa kila mlalamikiwa kwa kuwa hana uwezo wa kulipa Sh15 milioni zilizotajwa kwa mujibu wa sheria ya kesi za uchaguzi kwa mtu anayepinga matokeo.
Baada ya uamuzi huo kutolewa, alisema anakubaliana nao na yupo tayari kulipa kiasi hicho cha fedha ili kesi ya msingi aliyoifungua mahakamani iweze kusikilizwa na kutolewa hukumu.
Katika maombi yaliyowasilishwa na Wakili Msyani kwa niaba ya Wakili Daniel Lunyemela ambaye hakuwapo mahakamani, aliiomba Mahakama ikubali ombi la mteja wake kwamba, hataweza kumudu kulipa kiasi kilichokuwa kikitakiwa cha Sh15 milioni.
Msyani aliiambia Mahakama kuwa kutompunguzia gharama mteja wake ni kumnyima haki ya kupinga matokeo ya uchaguzi katika chombo cha sheria kama ilivyoainishwa.
Upande wa utetezi uliowakilishwa na mawakili waandamizi wa Serikali, Juma Masanja na Kennedy Fungamtama, waliiomba Mahakama itupilie mbali maombi hayo kwa madai kuwa Kafulila ana mali na fedha ambazo alilipwa zaidi ya Sh200 milioni na kwamba, alikuwa akilipwa na Bunge kila mwezi Sh11 milioni.
KAFULILA ATAKIWA KULIPA MILIONI 7.5 KAMA DHAMANA YA KESI YAKE YA KUPINGA MATOKEO YA UBUNGE
Reviewed by Unknown
on
9:44 AM
Rating: