STORY MPYA

recent

KATIBU MKUU TAMISEMI AKAGUA MIUNDOMBINU YA MFUMO WA MABASI YAENDAYO HARAKA


Katibu Mkuu Ofisini ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Jumanne Sagini (kushoto) akimweleza jambo Mwenyekiti wa Kampuni ya UDA-RT, Bw. Robert Kisena wakati alipofanya ziara kwenye miundombinu ya mfumo wa Mabasi yaendayo haraka kabla kipindi cha mpito hakijaanza mwezi ujao mwisho mwa wiki. UDA-RT ndiyo kampuni itayotoa huduma ya usafiri katika kipindi hicho na tayari imeshanunua mabasi 140.
WATOA huduma katika kipindi cha mpito cha mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam, kampuni ya UDA-RT wameihakikishia serikali na wananchi kuwa matayarisho yanaendelea vizuri tayari kwa huduma hiyo kuanza Januari 10 mwakani.

Ahadi hii ilitolewa wakati wa ziara iliyofanywa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini, alipokuwa akikagua miundombinu katika mabasi yanayotarajiwa kutoa huduma hiyo.

Siku chache zilizopita, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwataka wahusika wote wa mradi huo kuhakikisha unaanza mara moja ili kupunguza adha ya usafiri Dar es Salaam.

“Tulitaka kujiridhisha kama mabasi haya yako tayari kutoa huduma hii,” alisema Sagini mbele ya waandishi wa habari na kuwataka wahusika kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa haraka.

Mabasi 140 yanayomilikiwa na kampuni ya UDA-RT yatatumia mfumo wa kisasa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa ukusanyaji nauli, mifumo ya utoaji taarifa na maeneo maalum ya wazee na walemavu.

Mwenyekiti wa UDA-RT, Robert Kisena aliwataka wananchi kujali mabasi hayo mara huduma itakapoanza.

“Wananchi wajali mabasi haya, madereva nao wana wajibu wa kuhakikisha magari haya yanadumu,” alisisitiza.

Alisema kuhujumu mabasi hayo mapya au miundombinu ya mradi huo ni sawa na wananchi kujihujumu wenyewe, kwani huduma hiyo ni kwa ajili yao.

Alisema tayari kazi ya kufunga vifaa vinavyotakiwa katika mabasi hayo imeshakamilika kwa baadhi ya mabasi na inaendelea kwa mengine.

Msemaji wa UDA-RT, Said Mabruk alisema magari yote yanayotakiwa kuanza kwa huduma hiyo ya mpito yana madereva na walishapewa mafunzo na kwamba ni matumaini yao kuwa huduma itaanza kwa wakati uliopangwa.

Awamu ya kwanza inahusisha kilometa 20.9 za njia maalumu kutoka Kimara hadi Kivukoni, barabara ya Msimbazi kutoka Faya hadi Kariakoo- Gerezani na sehemu ya barabara ya Kawawa kutoka Magomeni hadi njia panda eneo la Morocco.
KATIBU MKUU TAMISEMI AKAGUA MIUNDOMBINU YA MFUMO WA MABASI YAENDAYO HARAKA Reviewed by Unknown on 7:09 AM Rating: 5
All Rights Reserved by TANZANIA COUNTRY BLOG © 2014 - 2015
Designed by JOJOThemes

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.