MAWAZIRI WA JK WATAJWA KUHUSIKA UFISADI WA MABILIONI
Watu tisa wakiwamo mawaziri wawili wa Fedha wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Jakaya Kikwete wametajwa kushiriki kwenye kashfa ya rushwa ya Sh13 bilioni wakati Serikali ya Tanzania
ilipokopa. Dola za Kimarekani 600 milioni (Sh1.3 trilioni) kutoka benki ya Standard ya Uingereza.
Ripoti ya Taasisi ya Kuchunguza Ufisadi (SFO) ya Uingereza iliyokuwa inafuatilia kashfa hiyo imewataja maofisa hao kuwa ni Waziri wa Fedha ambaye alifukuzwa kazi Mei 2012, na Waziri wa Fedha aliyefariki dunia Januari 2014.
Waziri wa Fedha aliyefukuzwa kazi Mei 2012 alikuwa Mustafa Mkulo wakati aliyerithi nafasi hiyo na baadaye akafariki akipatiwa matibabu Afrika Kusini Januari 2014 alikuwa Dk William Mgimwa.
Wakati ilipowasilisha barua ya pendekezo la mkataba wa mkopo wa Dola za Kimarekani 600 milioni (Sh12 trilioni) wizarani, Februari 2012, wizara ilikuwa chini ya Waziri Mkulo na mazungumzo ni kama yalififia kwa muda kabla hayajaanza upya Septemba chini ya Dk Mgimwa.
Kipindi cha uhai wake na kudumu kwake wizarani hapo, ripoti ya SFO iliyowasilishwa katika mahakama ya Southwark Crown ya jijini London, Uingereza inasema Dk Mgimwa ndiye aliyeidhinisha kuzinduliwa kwa hati fungani hiyo pamoja na nyaraka nyinginezo.
Mbali ya mawaziri hao, wengine waliokuwamo kwenye timu ya Serikali ya majadiliano ni Ofisa mwandamizi wa Hazina ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Madeni ya Serikali (NDMC). Huyo ndiye aliidhinisha barua ya ada ya mkataba na ile ya mamlaka.
Pia, alikuwamo msaidizi wa ofisa mwandamizi (Msajili wa Hazina) ambaye alipokea barua ya mapendekezo ya mkataba na waraka wa mamlaka kutoka Stanbic. Alihusika pia katika mapendekezo yaliyopitiwa na Waziri Mkulo.
Kamishna Msaidizi na Mshauri wa Sera wa wizara, alipokea barua ya mapendekezo ya mkataba na barua ya mamlaka kutoka Stanbic. Mwenyekiti wa Ufundi wa Kamati ya Madeni ya Serikali (TDMC) alipokea mapendekezo ya barua ya mamlaka na ile ya ada ya mkataba.
Hao ndio walikuwa wanakutana na timu ya maofisa wanne kutoka benki ya Stanbic. Kiongozi wa timu ya Stanbic alikuwa Bashir Awale, ambaye kwa wakati huo alikuwa mkurugenzi mtendaji wa Stanbic. Ingawa ripoti inamtaja kama alifukuzwa kazi Agosti 19, 2013 baada ya kushindwa kutoa ushirikiano wakati wa uchunguzi wa kesi hii, lakini inafahamika kuwa aliacha kazi mwenyewe.
Mwingine alikuwa Shose Sinare, ambaye alikuwa kaimu mkuu wa uwekezaji wa benki hiyo. Alikuwa anawajibika moja kwa moja kwa Bashir na alikuwa kiungo muhimu katika mkataba huu akimjuza mkuu wake kila lililojiri. Alijiuzulu Juni 3, 2013 na hivyo akawa amekwepa uchunguzi.
Ofisa wa tatu ametajwa kuwa ni mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Fedha (Mgimwa) aliyefariki dunia 2014. Mtoto huyo, kwa mujibu wa ripoti ya SFO ni mhitimu aliyekuwa kwenye mafunzo ya kazi.
Mtoto wa waziri huyo, Godfrey Mgimwa, ambaye sasa ni mbunge wa Jimbo la Kalenga, Iringa alipoulizwa jana kama amewahi kufanya kazi katika benki ya Stanbic alikiri kuwa kwa wakati huo alikuwa akifanya kazi katika benki hiyo, lakini hajui chochote kuhusu mchakato huo.
“Nimesikia habari hizo lakini sifahamu lolote. Kuwa mtumishi wa Stanbic wakati tukio hilo linatokea haimaanishi kuwa watumishi wote walihusika. Nadhani ni uhusiano uliopo kati yangu na waziri ndio unafanya nihusishwe…ni vile tu hatupo naye hivyo hakuna wa kuelezea zaidi. Kwa kuwa mzee amefariki naona inatafutwa namna ya kutengeneza uhusiano uliokuwepo kati ya taasisi zilizohusika,” alisema Godfrey.
Mtu wa nne kwa upande wa Stanbic alikuwa mkuu wa huduma za sheria na usuluhishi wa benki hiyo. Ingawa hakuwa sehemu ya mpango huo lakini alishirikishwa na alifukuzwa kazi Oktoba 31, 2013 baada ya kushindwa kufuata maagizo ya bodi ya wakurugenzi ya kutoa taarifa juu ya ushiriki wa kampuni ya Egma.
Tukio la kwanza kuwakutanisha wahusika wengi waliotajwa ni mkutano kati ya wawakilishi wa benki ya Standard, Stanbic na Waziri Mgimwa Mei 28, 2012 kujadili pendekezo la mkopo wa Dola za Kimarekani 550 milioni na siyo Dola 600 milioni. Bashir na Sinare waliiwakilisha Stanbic.
Siku chache kabla ya mkutano huu, Bashir alikuwa ametuma barua wizarani hapo akifafanua na kubadili baadhi ya vipengele vya pendekezo la mkataba wa Februari 2012. Katika barua hiyo, alieleza kuwa endapo wizara ingeendelea na mpango huo basi mkataba wa mkopo na nyaraka nyingine za kisheria ziwe kati ya wizara na serikali na si mamlaka nyingineyo.
Siku chache baada ya mkutano huo, Dk Mgimwa alimtuma mwanaye na kumpatia barua ya utambulisho kwa mkurugenzi wa Stanbic. Bashir aliahidi kuwa angemsaili yeye mwenyewe. Alikutana naye Julai na akaidhinisha kuajiriwa kwake chini ya mpango wa wahitimu walio kwenye mafunzo ya kazi na kukabidhiwa kwa vijana walioongozwa na Shose Sinare. Kwenye mchakato huo, inaelezwa kuwa mtoto huyo wa waziri alikuwa na ushiriki fulani mdogo uliofanikisha mkataba huo.
Waziri Mgimwa, Msajili wa Hazina pamoja na msaidizi wake wakiwa na aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mwenyekiti wa Bodi ya Egma, Harry Kitillya walisafiri kama ujumbe wa Tanzania ulioshiriki mkutano wa wawekezaji kwa lengo la kunadi pendekezo la kuuza hati fungani hiyo ambao uliandaliwa Benki ya Standard. Mkutano huo ulifanyika Februari 2013 na akihudhuriwa pia na Bashir na mwakilishi wa Standard.
Haya yamewekwa wazi na ripoti hiyo ya SFO yenye kurasa 55 ambayo ni matokeo ya uchunguzi wa ndani uliofanywa na mwanasheria wa benki ya Standard ya Uingereza, Jones Day. Baada ya uchunguzi huo Day aliwasilisha SFO ushahidi wote wa kimaandishi, baruapepe, simu na mazungumzo mengine aliyokusanya ya wote waliohusika na ukiukwaji wa taratibu za kibenki. Ripoti hiyo iliyotolewa Novemba 25, ndiyo imetumiwa na SFO katika shauri lililoendeshwa kwa mfumo wa mtindo wa makubaliano ya kumlipa fidia mlalamikaji (DPA) kwenye mahakama ya Southwark Crown ya jijini London, Uingereza.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo hadi Februari 2012 mapendekezo yalikuwa riba ya mkopo huo iwe asilimia 1.4. Baada ya Mukulo kuondolewa Sinare aliwahakikishia maofisa wa benki ya Standard ya Uingereza kwamba japokuwa hati ya uthibitisho ilikuwa haijatiwa saini “dili letu liko salama kwa sababu Serikali inahitaji fedha na dili letu linaungwa mkono na timu ya ufundi pamoja na maofisa waandamizi serikalini.”
Dk Mgimwa alipoiingia Mei 2012 mazungumzo yalizorota lakini yalipofufuliwa Septemba 2012 riba ilipandishwa hadi asilimia 2.4 kwa maelezo kuwa asilimia moja ni kwa ajili ya wakala wa Tanzania kampuni ya Egma (Enterprise Growth Markets Advisors Limited).
Benki zote mbili yaani Standard ya Uingereza na Stanbic zilijulishwa na Serikali ilifahamishwa.
Waliosimamia kidete ongezeko la asilimia hiyo moja ni Awale na Sinare. Novemba 2012 yaani miezi miwili baada ya kuipenyeza Egma katika mpango huo na kuilipa asilimia moja, ndipo Serikali iliwasilisha rasmi barua yake kwenye benki ya Standard na Stanbic ya mkopo wa Dola 550 milioni. Hadi mkataba huo unakamilishwa Machi 2013 kiwango cha mkopo kiliongezeka hadi Dola 600 milioni.
Stanbic ndiyo iliilipa Egma Dola 6 milioni (Sh12 bilioni) ambapo Mkurugenzi mtendaji wake Dk Fratern Mboya alizichota katika mikupuo minne kati ya Machi 18 na 27, 2013.
Ufisadi huu umeishtua Serikali ambapo juzi Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema Serikali imeanza kuzichunguza benki ya Stanbic na Egma kutokana na kuhusika katika udanganyifu wa riba ya mkopo huo. Tayari Stanbic imekubali kurejesha fedha hizo.
MAWAZIRI WA JK WATAJWA KUHUSIKA UFISADI WA MABILIONI
Reviewed by Unknown
on
1:19 PM
Rating: